Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wamefanyiwa mafunzo ya siku tatu lengo likiwa ni kujengewa uelewa wa mpango wa kunusuru Kaya maskini (TASAF awamu ya tatu) yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya kuanzia tarehe 07/05 hadi 09/05 ambapo mafunzo hayo yalifunguliwa na mgeni rasmi Bw.William Makufwe ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Mafunzo hayo yalifanyika kwa makundi ambapo siku ya kwanza yalifanyika kwa wakuu wa idara,vitengo na sehemu, siku ya pili yalifanyika kwa waheshimiwa madiwani , Mbunge na viongozi wa CCM Wilaya na siku ya tatu yalifanyika kwa watalaamu wa Halmashauri makao makuu na ngazi na Kata.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe amewaeleza Wataalamu kuwa lengo la TASAF kuja kwenye jamii zetu ni kuona namna ya kuwezesha Kaya maskini kuweka akiba na kubuni miradi mbalimbali ya mtu binafsi au ya kikundi ili kutoka kwenye Kaya maskini kwenda kwenye Kaya zenye unafuu na kwamba ifike hatua Kaya zisiwe maskini daima ziwe Kaya yenye uwezo wa kukidhi mahitaji yao .
Ameongeza kuwa TASAF watabaki kuwa wawezeshaji lakini shughuli zote zinaratibiwa na kusimamiwa na viongozi wa Halmashauri hivyo kila mtu anapaswa kujua nini anatakiwa kufanya kwa nafasi yake katika kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa ndiyo maana kuna wataalamu wa kila taaluma katika mafunzo haya ya kujengewa uwezo wa mpango huu wa kusuru Kaya Maskini yaani TASAF awamu ya tatu “Kila moja ajue anawajibu katika kufanikisha mpango huu” alisema.
Alihitimisha kwa kuwashukuru viongozi wa TASAF makao makuu kwa kuleta mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwani kwa Mkoa wa Tanga Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ndiyo Halmashuri pekee iliyopata mradi huo.
Naye Mratibu wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu kuweka akiba na kukuza uchumi wa Kaya kutoka TASAF makao makuu Bw.Hamisi Kikwape amewaeleza wawezeshwaji kuwa lengo la mafunzo hasa ni kukumbushana na tangu TASAF ianze kwa kitu chochote ambacho kinakianzishwa lazima viongozi wafanyiwe uelewa wa namna ya kuteleza shughuli husika ili utekelezaji unapofanyika kila moja anafahamu.
Amesema dhana ya TASAF awamu ya tatu ina vitengo vinne ambavyo ni uhawishaji fedha au ugawaji fedha kwa kiasi kilichokubaliwa katika Kaya ambayo inahusisha ruzuku ya masharti kama fedha za shule na matibabu, ajira za muda ambayo itampatia mlengwa kipato ambapo ajira ya muda imetekelezwa katika Halmashauri 44 nchi nzima. Kitengo kingine ni kuweka akiba na kukuza uchumi wa Kaya ambayo ina lengo la kuandaa mazingira ya Kaya maskini kuweka akiba na kubuni shughuli za kiuchumi ambazo zitawasaidia kuwa na hali nzuri za kiuchumi na kujitegemea hata baada ya TASAF kuondoka au baada ya walengwa kutoka kwenye mpango.
Sehemu ya tatu ni kuboresha miundo mbinu ambapo hii inatokea pale walengwa wanashindwa kutekeleza ruzuku ya masharti kwamba walengwa wanashindwa kupata elimu au matibabu kutokana na uhaba wa madarasa au hospitali hivyo jamii husika inatengeneza maombi na kutuma TASAF kwa kupitia hatua zote zinazotakiwa kupita kwaajili ya kupata fedha za kutekeleza ujenzi wa miundo mbinu hiyo. Sehemu ya mwisho ni kujenga uwezo katika mikakati mbalimbali ya kutekeleza mradi kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji na kwamba walengwa wanatakiwa kueleweshwa namna ya kutumia fedha,biashara ya kufanya,faida itakayotokana na mradi,kitu gani walengwa hawapaswi kufanya,nini wanapaswa kufanya na namna gani ya kufanya katika kila hatua ya mradi husika na pia kufanya ufuatiliaji wa jinsi shughuli zilivyofanyika.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa