Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wamefanya kikao leo na kamati ya usimamizi wa ujenzi wa kituo cha Afya kilichopo katika Kata ya Kabuku ambacho kinajengwa kwa fedha ya (Force occount) kiasi cha shilingi milioni mia nne,kamati hizo ni kamati ya Manunuzi,Kamati ya ujenzi na uhamasishaji na kamati ya mapokezi na ulinzi. Majengo yanayojengwa ni maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, nyumba ya mganga, chumba cha kufulia na chumba cha kuhifadhia maiti.
Katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.Ramadhani Diliwa amewaeleza wanakamati kuwa washirikiane katika kazi ya kufanikisha mradi kukamilika kwa wakati kwani tumepata fursa hivyo hatuna budi kutumia vizuri ili kukuza hadhi ya mji wetu wa Kabuku na kwamba tusiingize umimi katika kazi hii kila mtu afanye kazi kwa nafasi yake.
Aidha amewahimiza viongozi wa Kata kuwa pale inapohitajika nguvu za wananchi ifanyike hivyo kwani ndivyo mradi unavyotaka kwa hiyo wananchi wahamasishwe ili wajitokeze kwa wingi na kwamba mafanikio yetu ni mradi kukamilika na kuhudumia wananchi . Ameongeza kwamba mradi siyo wa mtu binafsi bali ni wa Kabuku yote na utawasaidia wananchi wote, alisema”tutokeni tukafanye kazi”.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe amezitaka kamati hizo kutoa taarifa ya matumizi kila baada ya wiki mbili kwenye kamati ya Kata na pia kwenye mkutano wa hadhara ili wananchi wajue maendeleo ya mradi na kwamba kamati ya manunuzi na kamati ya mapokezi zikae kila baada ya siku tatu ili waandae taarifa kwa pamoja kwaajili ya kusomwa kwenye vikao hivyo. Aidha amesisitiza leja ya kujaza vifaa kuwepo mahali ambapo vifaa ya ujenzi vinahifadhiwa kwaajili ya kujaza idadi ya vifaa vinavyoletwa na vinavyotumika na pia kuhakikisha leja hizo zinajazwa kwa wakati .
Pia amewahimiza viongozi wa Kata kuleta watu wasiopungua kumi na tani(15) kwa kila kijiji kila siku kuongeza nguvu kazi ya kutosha ili mradi ukamilike kwa wakati. Aliongeza kuwa kamati zifanye kazi zao bila kuingiliana majukumu ili kila moja iweze kufanya kazi kwa uhuru.Lakini pia aliwataka wanakamati kutomvumilia fundi ambaye hatafanya kazi kwa weledi na kwa wakati na kwamba inapotokea hali kama hiyo apewe onyo na akiendelea hivyo aondolewe mwingine awekwe ili mradi ukamilike kwa wakati na kuhudumia wananchi hasa akina mama.
MWISHO
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa