VIONGOZI WA JAMII NA WATOA HUDUMA YA AFYA YA MSINGI WAPEWA SEMINA KUHUSU SARATANI YA MATITI
Viongozi wa jamii pamoja na watoa huduma ya afya ya msingi katika ngazi ya jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, wamepatiwa semina maalumu kuhusu Saratani ya Matiti.
Akifungua semina hiyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Dkt. Kisaka Kachua, alisema mafunzo hayo yatasaidia watoa huduma kupeleka elimu kwa jamii, kuhamasisha uchunguzi wa mapema, na kubadilisha mitindo ya maisha ili kujikinga na saratani.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi, wanajitokeza mapema vituoni, na kuchunguzwa viashiria vya saratani ili kupata tiba kwa wakati,” alisema Dkt. Kachua.
Kwa upande wake, Mratibu wa Uhamasishaji na Uelimishaji wa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Bi. Elizabert Shengovi, alisisitiza umuhimu wa wanawake na wanaume kwenda kupima mara kwa mara ili kugundua viashiria vya saratani katika hatua za awali.
“Uchunguzi wa mapema unarahisisha kugundua ugonjwa katika hatua za mwanzo na hivyo kuanza matibabu mapema,” alisema Bi. Shengovi.
Aidha, mdau wa maendeleo, Arnold Japiego, alisema uelewa wa jamii kuhusu uchunguzi wa mapema utasaidia kupunguza vifo vinavyosababishwa na Saratani ya Matiti.
Semina hiyo inatarajia kuongeza mwamko kwa wananchi wa Handeni kujitokeza kwa wingi kupima saratani ya matiti, hatua itakayosaidia kupunguza maambukizi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa