Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa viongozi wote wabadhilifu wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwani wanakwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ameyazungumza hayo kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kwa kujitolea katika ujenzi wa miundombinu ya madarasa iliyopo kwenye maeneo yao kwa maenedeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mh. Gondwe alisema kuwa Ofisi ya Mkurugenzi imebaini baadhi ya viongozi kutumia vibaya fedha zilizotolewa kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Kiva na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji kumsimamisha kazi Mkuu wa Shule hiyo kwa kuzidisha bei ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa madarasa kulingana na bei iliyopo sokoni.
“Mwalimu huyu asimame kazi kwanza na mkaguzi wa ndani natoa siku 7 awe amemaliza kuchunguza taratibu za manunuzi na yeyote atakayebainika kuhusika kwa namna yeyote hatua za kinidhamu zitachukuliwa, fedha ya Serikali haichezewi” alisema Gondwe.
Aliongeza kuwa maendeleo hayataletwa na wananchi kutoka nje ya Handeni na kuwataka viongozi na wananchi kuwa na nidhamu na fedha zinazoletwa kwaajili ya kuboresha shule kwa manufaa ya watoto wao, na kwamba wao kama wananchi wanao wajibu wa kushiriki kwenye ujenzi wa miundombinu badala ya kuachia fedha inayoletwa na Serikali kufanya kazi pekee.
Aliongeza kuwa viongozi lazima wasimamie matumizi ya fedha na kuwashirikisha wananchi kwa kila fedha inayoingia na matumizi yake ili kuweka uwazi kwa wananchi na kujua kinachoendelea ili kuwapa motisha ya kuendelea kujitolea kwenye ujenzi wa miundombinu.
Aidha amewataka kupanga ratiba ya ushiriki wa Kila kitongoji kwenda kusaidia mafundi ili miradi inayojengwa iweze kuisha kwa wakati na kusaidia kupunguza gharama ili fedha zitakazobakia zitumike kwenye ujenzi wa miundombinu mingine kama maabara, nyumba za walimu na zahanati.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe amesema kuwa shule ya Kiva Sekondari na shule ya Msingi Kwechigwe fedha zimeletewa na Serikali Kuu kiasi cha Milioni 66 kwaajili ya ujenzi wa madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo.
Aliongeza kuwa ili kuboresha mazingira matundu ya vyoo yameongezwa na kuwa 18 na kuongeza ofisi moja ya waalimu kwa kila shule ili kuboresha zaidi miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, Hivyo hatutakua tayari kumvumilia mtumishi anayekwenda kinyume na taratibu.
Hata hivyo fedha hizo zinatumia utaratibu wa ushirikishwaji wa wananchi na kutoa nafasi ya ajira kwa vijana ambapo ametafutwa fundi mtaalamu na uongozi wa shule unanunua vifaa vya ujenzi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa