Serikali Wilayani Handeni imewahakikishia wachimbaji wadogowadogo wa madini ya dhahabu zaidi ya 100 waliopo katika Kijiji cha Kwamsampa Kata ya Kwasunga kwamba hawataondolewa kwenye machimbo hayo iwapo watafuata taribu na kanuni walizowekewa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe Mwishoni mwa Wiki alipowatembelea wachimbaji hao na kutoa maagizo ambayo lazima wayafuate kwa usalama wao ikizingatiwa eneo hilo ni la Kijiji na hakuna Mchimbaji Mkubwa yeyote mwenye lesene ya uchimbaji wa madini katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya aliwaeleza wachimbaji hao kuwa waendelee kuchimba kwenye machimbo hayo kwa kufuata taratibu za uchimbaji wa madini, wajiweke kwenye kundi kwa kuwa na daftari la majina yao ambalo litafuata taratibu za upatikanaji wa leseni na hatimaye kuwa na leseni halali ya wachimbaji wadogowadogo.
Gondwe Aliwataka wachimbaji hao kuacha kukata miti kiholela na badala yake wakate kwa ustaarabu ili waendelee kutunza rasilimali ya miti iliyotunzwa na wanakijiji wa eneo hilo kwa muda mrefu.Amewaeleza kuwa ni lazima wao kama wachimbaji wa Kata ya Kwasunga kutoa ushirikiano na kuheshima mamlaka ya Kijiji hicho kwa kufuata taratibu watakazopewa.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni William Makufwe amewaeleza wachimbaji hao kuwa kile kitakacho zalishwa lazima 20% iende Serikali ya Kijiji na 80% ibaki kwa wachimbaji wenyewe ili kila mmoja pate haki yake kwa utaratibu kwakuzingatia eneo ni mali ya Kijiji.
Afisa madini Mkazi Wilayani Handeni Frank Makyao ameeleza kuwa ili watambulike kama wachimbaji wa madini ni lazima waunde kikundi ambacho kitasajiliwa na kufika ofisini kwaajili ya kuwekwa kwenye mtandao ambapo itakuwa rahisi kuchukua kona nne na kupata kibali rasmi cha wachimbaji wadogowadogo.
Kamanda wa Polisi Wilayani Handeni William Nyelo amewataka wachimbaji hao kuhakikisha kuwa wanaimarisha usalama wao kwa kutoa taarifa polisi mara tu watakapoona uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na kutoruhusu wageni kuingia kwenye eneo lao kiholela na kwamba watumie uhuru waliopewa na Serikali kihalali.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa