Kongamano la wachimbaji wa madini Wilaya ya Handeni mkoani Tanga lililojumuisha wataalamu mbalimbali wa Halmashauri, wataalamu wa madini, Mamlaka ya mapato Tanzania, taasisi za fedha, wakala wa barabara za mijini na vijijini,wakala wa misitu, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na wachimbaji wenyewe limefikia maazimio baada ya kila moja kutoa changamoto zinazokabili maendeleo ya sekta hiyo Handeni.
Kongamano hilo lilifanyika tarehe 07-05-2019 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Mwl. Boniphace Maiga.
Akitoa maazimio hayo Mwl. Boniphace alisema wachimbaji wa madini wanatakiwa kufuata sharia, kanuni na taratibu za uchimbaji ikiwepo kufanya tathmini ya mazingira ya maeneo ya migodi na kwamba ndani ya mwezi moja taarifa ya tathmini iwe imetolewa ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Azimio lingine ni uanzishwaji wa umoja wa wachimbaji madini wa Wilaya ya Handeni na amesema ndani ya siku 60 huo umoja uwe umeshaundwa kwa kuwa kupitia viongozi wa umoja huo upatikanaji wa taarifa utarahisishwa. Amesema wachimbaji au makampuni yaliyowekeza yahakikishe pia yana mikataba ya wajibu wa makampuni kwa jamii na mikataba hiyo iwasilishwe ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kupitishwa na pia kwaajili ya ufuatiliaji na amewaagiza hadi tarehe 17-05-2019 wawe wameshawasilisha.
Aidha amesema makubaliano yafanyike kati ya wasafirishaji na wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) kuhusu matumizi ya barabara ili kuepusha malalamiko. Mwl. Boniphace ameitaka ofisi ya madini kutoa takwimu za uzalishaji wa madini za kila mwezi kwa kila Halmashauri ili ushuru wa huduma uweze kutolewa.
Pia amewataka wawekezaji na makampuni kutumia walinzi wanaotambulika au jeshi la akiba waliopewa ithibati na mkuu wa jeshi la akiba na kwamba kumtumia mtu ambaye hajapitia kwenye masuala ya ulinzi kwa taratibu zinazotambulika ni kosa kisheria na wafanyakazi wote wanaofanyakazi katika maeneo yao wachukuliwe taarifa zao kama ambavyo zinatambulika katika mamlaka mbalimbali za usajili ikiwepo anuani zao na namba za simu za ndugu zao.
Alihitimisha kwa kuwataka wachimbaji wa kati na wadogo kuhakikisha suala la ulinzi na usalama katika maeneo yao linaimarishwa pamoja na kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro, wadau hao pia waliaswa kutoa elimu kwa jamii ili kutoa taarifa za wageni wanaoingia katika maeneo ya migodi.
Wadau hao kwa pamoja walikubalibaliana kufanyika kwa kongamano la wadau wa madini Handeni mara mbili kila ili kuboresha sekta hiyo Wilayani Handeni.
MWISHO.
Mgeni rasmi Mwl.Boniphace Maiga akizungumza katika kongamano la wachimbaji wa madini.
Mgeni rasmi Mwl.Boniphace Maiga akikagua madini ya Handeni yaliyokuwa yanaonyeshwa kwenye kongamano.
Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji (Keneth Haule wa kulia aliyeshika jiwe) na Halmashauri ya Wilaya Bw.William Makufwe kushoto wakiangalia aina za madini.
Kamati ya Ulinzi na usalama ikikagua madini
Hayo ni baadhi ya madini yanayopatikana Handeni.
Wachimbaji wa madini wakitoa changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya madini Handeni.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa