Sikukuu ya wafanyakazi huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 01-05 kwa lengo la kufanya tatmini ya ufanyaji kazi wa watumishi ambapo kwa mwaka 2019 Wilaya ya Handeni imeadhimisha siku hiyo katika viwanja vya shule ya msingi Mkata vilivyoko Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe.
Mgeni rasmi Mh.Gondwe Gondwe katika maadhimisho hayo alitaka vyama vya wafanyakazi Wilaya Handeni kutoa taarifa kwa viongozi mapema pale wanapokutana na changamoto za wafanyakazi ili zitatuliwe mapema kwakuwa serikali iko tayari kushirikiana kwa jambo lolote la kujenga na kwamba wasisubiri mpaka siku ya maadhimisho ya wafanyakazi ndipo waseme.
Gondwe alitoa rai kwa wafanyakazi kuchukua mikopo katika taasisi za serikali kwani riba ya taasisi za binafsi ni kubwa sana na wakati mwingine baadhi ya wanafanyakazi wanakabidhi makadi yao ya benki kwa hizo taasisi kitu ambacho ni kinyume na sharia na kuwaomba viongozi wa wafanyakazi kuwaelimisha wafanyakazi hasa walimu kwakuwa wengi wao ndiyo wanaokabidhi makadi ya benki kwa hizo taasisi za binafsi na kujichukulia fedha za mfanyakazi wenyewe.
Aidha, aliwapongeza Wakurugenzi wakutoa zawadi za wafanyakazi bora kwa kuwapa vyeti na fedha taslimu bila kuwasubirisha na kuagiza kulipa madeni ya wafanyakazi bora ya zamani ndani ya mwezi huu wa tano.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Handeni Bw. Athumani Malunda aliwapongeza wafanyakazi kwa kufanyakazi kwa weledi pamoja na mazingira magumu waliyonayo na kuwaomba kuwa wazalendo, washirikiane wapendane na kufanyakazi kwa umoja.
Malunda amewataka wakuu wa idara kusilikiza kero za wafanyakazi na kuzitatua badala ya kutumia vyeo vyao kuwakandamiza wafanyakazi walio chini yao au kuwabagua “Mimi kama kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya sitakubali kuona wafanyakazi wanaonewa”Alisema.
Katibu Tawala Wilaya ya Handeni Mwl. Boniphace Maiga amesema upandishwaji wa madaraja unaendana na utendaji kazi wa mtumishi unaomridhisha mwajiri na amesema takwimu zinaonyesha utendaji kazi wa watumishi katika maeneo mbalimbali hauzidi kiwango cha 50% hivyo wajitahidi kufanya kazi kwa bidii na weledi na kwamba waajiri wazingatie vigezo vya upandishaji vyeo vilivyoainishwa kwenye barua bila kusahau watumishi wengine.
Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji (Bw.Keneth Haule) na Wilaya (Bw.William M. Makufwe) wamewashukuru watumishi kwa ushirikiano hadi kufikisha Wilaya ilipo na kuwasihi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kujitambua na kuwa wabunifu na wamesema madai yote ya wafanyakazi yameshapelekwa wizarani na yanafanyiwa kazi hivyo wawe na subira.
Mgeni rasmi Mh.Godwin Gondwe akizungumza na wafanyakazi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bw. Athumani Malunda akitoa nasaha.
Katibu Tawala Wilaya ya Handeni Mwl.Boniphace Maiga akitoa neno.
Moja ya mabango ya wafanyakazi
Burudani mbalimbali zilipamba shughuli.
Wafanyakazi bora wakipokea zawadi
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa