WAFUGAJI NA WANAFANYABIASHARA HANDENI WAAFIKIANA KUFUFUA MNADA WA MKATA
Wafanyabiashara na wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wamekubaliana kufufua mnada wa Mkata ambao uliacha kufanya kazi tangu mwaka 2013 kutokana na sababu mbalimbali ambazo hazikuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wafugaji hao kama vile namna ya utozaji wa ushuru, njia ya mifugo na alama za vivuko vya wanyama.
Maafikiano hayo yalifanyika jana katika kikao cha pamoja baina ya wadau hao na uongozi wa Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa Neema ulioko Kijiji cha Mkata Mashariki ambapo kwa pamoja walikubaliana mnada kufanyika kila jumatatu kuanzia tarehe 12/11/2018
Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya ya Wilaya ya Handeni Bi Rahel Mbelwa aliwasihi wadau hao kushirikiana kwa pamoja na kutokujadili yaliyopita kwani kwa kipindi hicho Halmashauri zilikuwa zinatumia wazabuni ambao hawakuwa watumishi wa Serikali hivyo hawakufuata kanuni,taratibu na sheria katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa kuwatoza watu isivyotakiwa ili kujipatia kipato kikubwa.
Aliongeza kuwa mnada wa Mkata utakuwa na faida kubwa kwa wafugaji na wafanyabiashara kwakuwa mji wa Mkata unakua na pia unafikika kwa urahisi na kwamba wanunuzi wa mifugo watakuwa wengi hivyo bei ya mifugo itakuwa nzuri ukilinganisha na minada mingine.
Pia alisema Mkata kuna benki ambayo itawarasishia wanunuzi na wauzaji kutotembea na fedha kwaajili ya usalama wao kwani kumekuwa na matukio ya kuporwa fedha kwa wafanyabishara kutokana na mazingira wanayofanyia kazi kutokuwa na benki na uwepo wa kituo cha Polisi Mkata utawafanya watu kufanya shughuli zao kwa usalama pia.
Naye Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Sekiara Kiariro alitoa ufafanuzi kuhusu mifugo ambayo haijauzwa kutozwa ushuru baada ya wafugaji kulalamika kutozwa ushuru huo, Alisema kwa kipindi hicho Halmashuri ilikuwa inatumia wazabuni ambao hawakuwa watumishi wa umma na walitoza uhuru usiostahili ili kufikisha malengo ya Mikataba yao na kwamba huo utaratibu sasa haupo tena kwani ushuru unakusanywa na watumishi wa Halmashauri wenyewe hivyo kuwahakikshia ushuru huo kutokuwepo tena.
Pia alitoa ufafananuzi kuwa ushuru wa mfugo ni shilingi elfu tano tuu na si zaidi ya hapo mpaka hapo ambapo Serikali itatoa waraka wa mabadiliko, kwa upande vibali vya kuuza mifugo vinavyotolewa kwenye vijijini alisema ni bure hivyo wafugaji wasije wakadanganywa kuwa kuna gharama ya kukata vibali vya kuuza mifugo lakini alitoa angalizo kwa wale wafugaji ambao hawatambuliki kwenye maeneo yao wahakikishe wanatambulika kwani kwa yeyote atakayeleta mifugo yake mnadani bila kibali hatatambulika. “hii inasaidia kuzuia wizi wa mifugo na uingiaji holela wa mifugo katika maeneo yetu”alisema.
Mtendaji wa Kata ya Mkata Bw. Athumani Ndutu aliwahakikishia wafugaji kutenga njia ya mifugo kupita ili kuepuka migogoro na kwa upande wa vivuko alisema tayari alama za vivuko vya wanyama zimeshawekwa.
Kiongozi wa wafugaji Handeni Bw.Shapati kwa niaba ya wadau hao alipongeza uongozi wa Halmashauri kwa kuitisha kikao hicho na pia kufikia muafaka wa kurudisha mnada wa Mkata kwani wanaamini watauza mifugo yao kwa bei nzuri kama ilivyokuwa awail bei ambayo hawakuipata kwenye minada mingine tangu mnada huo uvunjike.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa