Wanafunzi Wilayani Handeni wametakiwa kuichukulia michezo kuwa sehemu ya ajira rasmi kwa kuweka bidii zaidi katika michezo.
Rai hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Ndolwa na Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Mh. Joel Mabula alipokuwa akifungua kambi ya wanafunzi wanojianda na mashindano ya umoja wa michezo shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Tanga hivi karibuni.
Mabula aliwaeleza wanamichezo hao kuwa michezo ni muhimu sana kwa sababu ni ajira rasmi“ Michezo kwa sasa ni ajira sio tu kwa vijana wa kiume hata wakike, na sio kwa mipira ya miguu pekee, bali hata kwa michezo mingine kama riadha, mpira wa pete hivyo nawashauri vijana wangu kucheza michezo hii kwa juhudi ili baadae iwasaidie” Alisema Mh. Mabula.. Alisisitiza kuwa vipaji vimekuwa vikiibuliwa katika michezo ya UMISSETA na kuendelezwa hatimaye kupatiwa ajira rasmi.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa michezo ni muhimu kwa sababu inaimarisha afya ya mwili na akili. Alisema kuwa kutokanan na umuhimu huo wa michezo, vijana wamekuwa wakiimarika na kufanya vizuri katika msomo yao ya darasani kutokana na michezo kuwa na uhusiano na kufaulu katika masomo.
Mabula aliwataka wanamichezo hao vijana kuwasikiliza kwa makini walimu wao ili waweze kunufaika na elimu ya michezo waliyonayo walimu wao.Aidha, aliwataka kudumisha umoja na mshikamano ili kuweza kutwaa tunzo nyingi katika michezo hiyo.Vile vile aliahidi kuongeza mipira miwili kwa timu ya wavulana na wasichana ili kuongeza kasi ya mazoezi.
“ Naomba mkawe wawakilishi wazuri wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, mafunzo na maelekezo mnayopewa na walimu wenu yakawaongoze vyema katika kuelekea kupata ushindi,muige mfano wa kaka zenu Serengeti boys ambao wamefanikiwa kuwakilisha vyema Taifa kwa ushindi waliopata dhidi ya Gabon” alisema Mabula.
Wakati huohuo Mratibu wa michezo Wilaya ya Handeni Bw. Msafiri Mhando alisema kuwa matarajia yake ni kupata ushindi kwa timu zote nne (timu ya mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu na riadha) wanazoziandaa kwenda kuiwakilisha Halmashuri ya Wilaya ya Handeni.
“Tunapeleka timu zetu kwenda kushindana na kila timu tunatarajia kushinda kwani tunajiandaa vizuri na hii ndio itakuwa njia nzuri ya kuitangaza Wilaya yetu ya Handeni kimichezo” alisema Bw. Msafiri.
Kambi ya Mashindano ya UMISSETA Wilayani Handeni yameanza tarehe 19/5/2017.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa