Wananchi Wilayani Handeni wametakiwa kutunza vizuri chakula katika kipindi hiki cha mavuno na kuwaepuka wafanyabiashara walaghai wanaotaka kununua mazao yao kwa bei ya chini.
Rai hiyo ilitolewa na katibu Tawala Wilaya ya Handeni, John Mahali aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe katika maonesho ya wakulima yaliyoandaliwa na wazalishaji wa mbegu za SEED-CO Jana, walipotembelea shamba darasa la mahindi lililolimwa kwa kutumia mbegu za mahindi za SEED-CO kutoka kampuni ya The African Seed Company ya mjini Arusha katika Kata ya Kwamatuka Wilayani Handeni.
Mahali aliwataka wakulima kutouza mahindi mabichi yaliyopo shambani na hata baada ya kukauka yasiuzwe yote badala yake yabaki kwa hifadhi ya chakula. “Hakikisheni wafanyabiashara wasiwalaghai kwa kuuza mahindi kwa bei ya chini, kumbukeni kuwa mtahitaji kuwa na fedha za kununulia pembejeo kwa msimu wa kilimo utakapofika. Tunzeni mahindi yenu kwenye maghala kusubiri bei itakapokuwa nzuri ndio muuze” alisema Mahali.
Katibu Tawala Wilaya aliwakumbusha wananchi kuwa teknolojia ya kilimo inazidi kukula kila kukicha. Aidha, aliwashauri wakulima wilaayani hapa kwenda sambamba na kasi ya teknolojia ili kujihakikishia mazao bora kwa kutumia mbegu bora zinazotoa matokeo chanya.
“Kampuni ya African Seed wanaozalisha mbegu za mahidi za Seed-Co wana mbegu bora kama ambavyo tumeshuhudia kwenye shamba darasa muda mfupi uliopita. Ni vema wakulima mkatumia mbegu hizi kwa uhakika mkubwa wa chakula na kipato cha kutosha” alisema Mahali.
Aidha, aliwataka wakulima kutumia mbegu kutoka kwa mawakala waliopitishwa na Wilaya ya Handeni ili kuepuka mbegu zisizo na ubora. “Chukueni mbegu kwa mawakala waliopitishwa na kamati ya pembejeo ya Wilaya na mnaponunua mbegu nunueni zenye asilimia kati ya 90-100 ndizo zenye uhakika wa kutoa mazao kwa wingi” alisema Mahali.
Alisema wakati nchi inaelekea kuwa ya uchumi wa kati, wakulima wanawajibu wa kuongeza juhudi kwenye kilimo cha mazao ya nafaka kwa kutumia wataalamu wa kilimo waliopo ili waweze kuzalisha mazao ya kutosha kwa ajili ya kusaidia viwanda vya usindikaji nafaka na chakula.
Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuondoa ushuru wa pembejeo za kilimo. Alisema kuwa baada ya ushuru huo kuondolewa, bei ya pembejeo itashuka na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na kilimo.
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni inatarajia kuvuna Tani 90,000 za mazao ya nafaka kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017.
Baadhi ya wakulima wakishuhudia shamba darasa
Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni walionufaika na mbegu bora za mahindi za SEED-CO
Mgeni rasmi Bw. John Mahali wa kwanza kulia akipata maelekezo kutoka kwa Mtaalamu wa mbegu za SEED-CO Bw. Kassimu Nyaki.
Baadhi ya wataalamu wa Kilimo na mbegu za SEED-CO
Mgeni rasmi Bw. John Mahali akitoka kushuhudia shamba darasa akiwa ameongozana na wakulima na wataalamu mbalimbali.
shamba darasa lililopo kwa kwamatuku.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa