Wananchi Wilayani Handeni wametakiwa kutilia mkazo suala la kuwapeleka watoto kupata chanjo mara zinapotangazwa ili kuendana na msemo wa kinga ni bora kuliko tiba.
Rai hiyo ilitolewa wakati wa uzinduzi wa wiki ya chanjo ya polio wenye kauli mbiu ya “jamii iliyochanjwa ni jamii yenye afya” uliofanyika katika Zahanati ya Mumbwi iliyopo Katika Kijiji cha Mumbwi kata ya Komkonga.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe mbaye pia alikuwa mgeni rasi alieleza kuwa Serikali inajitahidi kutoa chanjo bure hivyo wananchi pia wanao wajibu wa kuhakikisha wanapeleka watoto wao kupata chanjo hizo kwaajili ya ustawi wa afya za watoto.
“Halmashauri ya Wilaya ya Handeni inazo chanjo za kutosha, chanjo mkoba na chanjo tembezi zitafika kwenye maeneo ambayo bado hayana zahanati ili kuhakikisha watoto wote Wilayani Handeni wanachanjwa” alisema Mh. Gondwe.
Aidha , aliwataka Maafisa Tarafa, Watendaji Kata na Vijiji kuweka agenda ya usafi na mazingira, afya na bima kuwa ndelevu katika viko vyao vya Vijiji.
Akizungumzia suala la malaria kwenye siku ya maadhimisho ya siku ya malaria duniani Mh. Gondwe alisema kila mwanachi anawajibu wa kutunza mazingira na kutokomeza mazalia ya mbu ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo.
“Chanjo zinatolewa bure,vipimo vya malaria vinatolewa bure na baadhi ya dawa za malaria bure lakini ni vyema kila mwananchi kuwa na bima ya afya ili kuepuka gharama za matibabu na kuhakikisha kuwa suala la afya haliwi tatizo kwenye Wilaya ya Handeni”alisema Mh.Gondwe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Simon Mdaki alieleza kuwa chanjo zingharamiwa hivyo ni vyema wananchi kutambua umuhimu wa kupeleka watoto kupata chanjo.mtoto akiuguwa wasikimbilie kuhisi mtoto kalogwa badala yake wamuwahishe hospitali ili kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa unaomsumbua. Polio sio ugonjwa wa kulogwa ni chanjo ndio inapaswa kupatiwa mtoto angaliakiwa mdogo.
Aidha aliwataka wananchi wote kuzingatia kinga na kutunza mazingira kutokomeza madimbwi na mazalia ya mbu huku wakizingatia matumizi bora ya vyandarua ili kujikinga na ugonjwa wa malaria.
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ilikuwa na lengo la kutoa chanjo kwa watoto 2883 badala yake wamechanja watoto 3435 sawa na asilimia 119 (kwa kipimo cha penta) mbali na changamoto mbalimbali zinazokabili Idara ya Afya.
Uzinduzi huo ulipambwa na kikundi cha ngoma za asili cha chanika kofi na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya wakiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mwenyekiti wa Chama CCM Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Handeni, Wataalamu wa Afya na watendaji wa Halmashauri.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa