Wananchi Wilayani Handeni wamehamasishwa kujikinga na magonjwa ya ngono na ukimwi,kutokomeza ukeketaji kwa watoto wa kike, kujikinga na ujauzito na ndoa za utotoni na athari zitokanazo na kutojifungulia kwenye vituo vya afya.
Uhamasishwaji huo umefanywa na shirika lisilo la kiserikali Amref Health Africa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuhusu afya na haki ya uzazi.
Akizungumza Afisa Mradi wa “Kijana wa Leo” Henry Bendera amesema kuwa lengo kuu la kufanya uhamasishaji huo ni kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha afya na haki ya uzazi na ujinsia kwa vijana na kinamama walio katika umri wa kujifungua.
Aliongeza kuwa mradi wa kijana wa leo unaelimisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni juu ya umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya,kujikinga na magonjwa ya ngono na ukimwi, athari za ujauzito na mimba za utotoni, athari za ukeketaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa kutumia makundi mbalimbali waliopo shuleni na nje ya shule ikiwa ni pamoja na kufanya matamasha yanayojumuisha wananchi wote.
Mratibu wa Afya ya mama na mtoto Wilayani Handeni Bi. Neema Kombo alisema kuwa takwimu kubwa inaonesha wamama hawajifungulii kwenye vituo vya afya hali inayopelekea kuongezeka kwa idadi ya wamama wanaopoteza maisha kutokana na kujifungulia kwenye maeneo ambayo si salama.
Aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wamama kujifungulia kwenye vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kupatiwa huduma za wali mara tu baada ya mama kujifungua kwa usalama wake na wa mtoto, pia alisema kuwa ni jambo la busara mama anapojihisi kuwa ni mjamzito kwenda hospitali kuanza kliniki mapema na kupata ushauri wa daktari juu ya ukuaji wa mtoto.
Kwa upande wake mratibu wa magonjwa ya ngono na ukimwi Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dk. Mbonea Yonaza alitoa rai kwa wananchi ngazi ya familia kuhakikisha wanapima virusi vya ukimwi ili kuepuka maambukizi mapya ambayo mama hakuwanayo kipindi cha ujazuzito na kukinga watoto kuambukizwa.
Aliongeza kuwa Serikali inadhamiria ifikapo 2025 kutokomeza kabisa virusi vya ukimwi ndio maana upimaji wa hiari unahamasishwa kwa wananchi wote ili asilimia 90 ya kila eneo husika wananchi wote wawe wamepimwa na kutambulika afya zao
Akizungumzia athari za ujauzito na ndoa za utotoni Afisa Maendeleo ya jamii Bi. Amina Waziri aliwataka wazazi kuacha tabia hiyo kwa kuwa kumuoza mtoto katika umri mdogo ni kukatisha ndoto za mtoto huyo kwani kila mtoto anandoto anazotaka kuzitimiza kupitia elimu kwa kuzingatia kuwa elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto.
Aliongeza kuwa ndoa za utotoni zinasababisha kuongezeka kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi,kuzorota kwa hali ya uchumi ngazi ya familia,mtoto kupata maradhi kama ya Ukimwi na wakati mwingine vifo wakati wa kujifungua kwa sababu viungo vyao vya mwili vinakuwa havijakomaa kukabiliana uzazi.
Afisa mradi msaidizi Ibrahim olekinwaa aliwaeleza wananchi athari za ukeketaji kwa watoto wa kike na kuwataka kuondokana na dhana potofu ya kwamba mtoto wa kike aliyekeketwa hawezi kuolewa sababu hajakamilika kwa kutokukeketwa.
Alieleza kuwa shirika la amref health Africa limeleta njia mbadala ya kusherehekea, kufanya shughuli zote za kimila na kuvusha rika watotowa kike kwa jamii zote za kimasai na wakulima bila kukeketa kwani kitendo hicho hakikubaliki duniani kote na kwamba ni kinyume cha haki za binadamu na ni unyanyasaji wa kijinsia.
Mradi wa Afya na Haki ya uzazi na ujinsia wa kijana wa leo ni mradi wa miaka mitatu, ulianza kutekelezwa octoba 2015 hadi septembba 2018 na kwa awamu ya kwanza unatekelezwa kwenye kata 12 kati ya kata 21 zilizopokwenye halmashuri ya wilaya ya handeni, mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa shirika la Amref Health Africa Tanzania na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Jumla ya kata 4 (Sindeni, Kwankonje, Kwachaga na Makata) zimehamasishwa kuhusu afya na haki ya uzazi kuanzia jumanne na kuhitimishwa ijumaa ikiwa na takribani ya watu 300 waliojitokeza kupima kwa hiari virusi vya ukimwi
Baadhi ya wananchi waliojitokeza
Mratibu wa mradi kutoka Amref Bw. Henry Bendera akielimisha wananchi
watoa maada walioketi viti vya mbele
Afisa Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Amina Waziri akielimisha wananchi.
Mratibu wa Afya ya mama na mtoto Bi. Neema Kombo akielimisha wananchi.
Mratibu wa magonjwa ya ngono na ukimwi Dk .Yonaza Mbonea akielimisha wananchi.
Afisa mradi msaidizi Ibrahim Olekinwaa akielimisha wananchi madhara ya ukeketeji
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa