Watendaji na wataalamu wa Wilaya ya Handeni wametakiwa kusimamia na kuweka suala la elimu ya madhara ya ukeketaji kuwa ajenda rasmi kwenye vikao vyao ngazi ya Kata na Tarafa ili kukomesha kabisa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike wa jamii ya wafugaji hususani pindi mradi wa “KIJANA WA LEO” unaofadhiliwa na shirika la Amref kukoma.
.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe ametoa rai hiyo leo alipohudhuria sherehe za uvushwaji rika wa wasichana 170 wa jamii ya wafugaji(Ndito) zilizofanyika Kata ya Malezi katika mtaa wa Kwamadule.
Mh. Gondwe alisema kuwa ni haki ya binti anapokuwa mtu mzima na kuvushwa rika asiweze kunyanyaswa kijinsia, kwasababu athari za ukeketaji zinafahamika ikiwa ni pamoja na kuwa ni kitendo ambacho ni kinyume na maagizo ya Mungu lakini pia uvunjwaji wa haki za binadamu..
Ameongeza kuwa jamii ya wafugaji inatamaduni zilizoshiba na wanachangia kwa kiasi kikubwa kuingizia pato na fedha za kigeni Taifa, ni utamaduni bora unaotambulisha Tanzania kwa zaidi ya makabila 120.Watu wanapenda tamaduni za kimasai na jamii za wafugaji wengine lakini mila ambazo ni potofu zinazoleta maumivu katika jamii zitokomezwe.
“ sherehe na kila kitu kifanyike, watoto wafundishwe lakini ukeketaji hapana ili tumuokoe binti huyu na maumivu makali kwa sababu morani wamekubali kuoa wananwake ambao hawajakeketwa na kwasasa wanaoa hata jamii zingine ambazo wanawake hawajakeketwa” alisema Mkuu wa Wilaya.
Aidha aliwataka wataalamu wote ngazi ya Tarafa Hadi vitongoji ikiwa ni pamoja na idara zote hususani Elimu na Mendeleo ya jamii kuendelea kutoa elimu na kubaini wale ambao bado wanaendeleza vitendo vya ukeketaji kwa siri ili kuchukua hatua za kisheria kwasababu wanakwenda kinyume na haki za binadamu na kisheria hairuhusiwi.
Meneja mradi wa Amref Health Africa Dk.Aisha Byanaku amesema kuwa lengo kuu la mradi ni kuborehsa afya ya uzazi kwa vijana ambao wako katika umri wa miaka 10-24 ambapo hadi sasa elimu kwa jamii ya wafugaji imetolewa ikiwa ni pamoja na mangariba, watoa huduma za afya na viongozi wa kimila.
Mradi wa “KIJANA WA LEO”ulizinduliwa na Amref Health Africa Wilayani Handeni Octoba 2015 ukifadhiliwa na Allen&Overy na big Lottery fund ambapo hadi sasa jumla ya wasichana 830 wamefanyiwa sherehe za kimila (kuvushwa rika) bila kukeketwa kwa Kata za Malezi,Msomera na Kwamagome za Wilaya ya Handeni.
Sherehe za uvushwaji rika zimehudhuriwa na wakurugenzi wa Handeni na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni akizungumza na jamii wa wamasai kwenye sherehe za uvushaji rika
Muuguzi wa kimasai akihamasisha wazazi kuwapeleka watoto shule na kuepuka ndoa za utotoni.
mmoja wa wazee wa kimila akishukuru kwa elimu iliyotolewa na Shirika la Amref Health Africa
mmoja wa wsichana waliovushwa rika bila kukeketwa akipokea cheti cha kufuzu mafunzo ya kuzuia ukeketaji na mafunzo ya afya ya uzazi
Mkuu wa Wilaya ya Handeni akizungumza na Mangariba na kuwapongeza kuelimika kuacha vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike
Mratibu wa mradi kutoka Amref Health Africa Dk.Aisha Byanaku akitoa maelezo na malengo makuu ya mradi wa KIJANA WA LEO
mangariba wakionesha namna ambavyo huwakamata wasichana (ndito) wa kimasai kuwapeleka kwenye chumba cha ukeketaji.
wasichana wakiimba wimbo wa kupinga ukeketaji mbele ya mgeni rasmi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa