Katika kuhitimisha juma la elimu ya watu wazima wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika lenye kauli mbiu ya “kujua kusoma katika ulimwengiu wa sayansi na teknolojia kwa maendeleo ya nchi”mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya amewataka wazazi kuwapeleka shuleni watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule.
Akizungumza kwenye Hitimisho la juma la Elimu ya Watu wazima jana lililofanyika Shule ya Msingi Kweditilibe Kata ya Kiva ,Afisa Tarafa ya Sindeni Bw. Sijaona Bugufi amewaeleza wazazi umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shuleni ili kuondokana na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika hapo baadae.
Aliongeza kuwa lazima tupunguze na kuondoa kabisa idadi ya watuwazima wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika ili kukuza uchumi wa jamii yetu na Taifa kwa ujumla, kwa maana taifa lolote lililoendelea lilianza na kuondoa ujinga miongoni mwa wananchi wake kwa kuwapa elimu.
Alisisitiza kuwa Elimu wanayopata watu wazima isiwe ya darasani tu, lakini pia ijikite kwenye ujasiliamali ili wazee wetu wajishughulishe katika shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato na kujenga uchumi wa taifa letu kwani ndani ya hizo shughuli ndogondogo ndipo kunapopatikana na viwanda vidogovidogo katika kuelekea uchumi wa viwanda.
Aliwaasa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo ya maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujitolea nguvu kazi kwenye ujenzi wa miundo mbinu iliyopo kwaajili ya manufaa ya vizazi vyao, ikiwa ni pamoja na Maabara, madarasa na nyumba za walimu.
“katika kupeleka gurudumu la maendeleo mbele lazima wote tushiriki nguvu kazi, natoa rai kwa wananchi maabara zilizoanzwa kujengwa zimaliziwe ili watoto wetu waweze kujifunza kwa vitendo na kuongeza ufaulu wa masomo yote ya sayansi” Alisema Bugufi.
Mwisho aliwaeleza wananchi kuwa changamoto zote zilizoanishwa kwenye Risala yao amezipokea na atazifikisha ofisini kwa Mkuu wa wilaya ili kuona ni namna gani ambavyo wanaweza kushirikiana kuzitatua kwa pamoja na kumtaka Mkuu wa Shule ya Msingi Kobil kuandika barua inayoainisha changamoto wanazokabiliana nazo na kufikisha ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Kwaupande wake Kaimu Mkurugenzi Bi. Nipael Ezekieli (Mwanasheria wa Halmashauri) aliwasisitiza watoto kusoma kwa bidii na kutumia fursa ya elimu bure ambayo Serikali inagharamia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wananchi wake wote wanapata elimu za Msingi.
Katika kupambana na mapambano dhidi ya wasiojua kusoma na kuandika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imeweza kuendesha madarasa 10 ya MEMKWA yenye wananfunzi wapatao 489 kati yao wavulana 312 wasichjana 177 na uwepo wa idadi hii umetokana na wanafunzi walioacha shule kwasababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na umbali wa shule, kuhamahama kwa wazazi na utayari duni wa wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao hali inayopelekea watoto hao kuacha shule na idadi ya wasiojua kusoma na kuandika kuongezeka .
Elimu inayotolewa kwa watuwazima mbali na kujua kusoma, kuhesabu na kuandika, elimu ya ujasiliamali, vikoba,kilimo na vikundi mbali mbali inatolewa ili kuwakwamua kichumi.
Juma la elimu ya watu wazima limeadhimishwa kuanzia tarehe 5-12 octoba 2017 badala ya tarehe 1-8 septemba sababu za kupelekwa mbele ni kufanyika kwa mitihani ya taifa ya darasa la saba na shughuli za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Juma hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Handeni huku mgeni rasmi akiwa ni Bw.Sijaona Bugufi afisa Tarafa ya Sindeni akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya Mh. Godwin Gondwe aliyekuwa na majukumu mengine.
Baadhi ya walengwa wa elimu ya watu wazima
Wanafunzi na wananchi walioshiriki kwenye maadhimisho hayo
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Bw. Sijaona Bugufi (Afisa Tarafa Sindeni) Akizungumza na wananchi kwenye maadhimisho
Wanafunzi shule ya Msingi Kweditilibe wakiongoza wimbo wa Taifa
Viongozi wakiimba wimbo wa Taifa
Mh.Diwani Kata ya Kiva Rajabu Kibwana akizungumza kama Diwani wa Kata, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mwenyekiti wa Hufuma za jamii
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Bw. Fikeni Senzighe akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Afisa Elimu ya Watu wazima Bw. Elibariki Mfinanga akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Kaimu Mkurugenzi Bi. Nipael Ezekiel( mwanasheria wa Halmashauri) akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa