Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kasim Mjaliwa Majaliwa alifanya ziara ya kikazi Wilayani Handeni Mkoani Tanga jana, lengo likiwa ni kuona utekelezaji wa shughuli za seriikali pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mh. Majaliwa alizungumza na wananchi wa Handeni katika miji midogo ya Michungwani, Kabuku, Mkata na viwanja vya shule msingi Chanika.
Akijibu kero za wananchi ikiwepo uhaba wa vituo vya afya na wataalamu wa afya, uhaba wa maji safi na salama, wawekezaji kumiliki mashamba makubwa bila kuziendeleza, barabara mbovu na ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji alisema serikali ipo kwaajili ya kuhudumia wananchi hivyo itatatua kero hizo kwa wakati ili waweze kuishi maisha bora.
Kwa upande wa vituo vya afya alisema serikali tayari imeshaanza kupeleka fedha katika Halmashauri ili kupunguza adha ya Hospitali za Wilaya kulemewa na alisema mwaka huu serikali itatoa ajira ya madaktari hivyo aliwatoa hofu wananchi kuwa madaktari Handeni wataletwa lakini kwa upande wa Zahanati aliwahimiza wananchi kuanzisha ujenzi wa majengo ya Zahanati na kuzielekeza Halmashauri kupitia mapato ya ndani kumalizia majengo hayo ili wananchi wweze kupata huduma karibu na maeneo yao wanayoishi.
Waziri Majaliwa alisema serikali pia imeshatoa fedha kwaajili ya ukarabati wa barabara lakini kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha hazitaweza kukarabatiwa lakini baada ya msimu wa mvua kuisha barabara zote zitakarabatiwa isipokuwa zile barabara zilizokata mawasiliano zinatakiwa zitengenezwe baada tu ya kuharibika bila kusubiri msimu wa mvua kuisha. Kwa suala la umeme amesema serikali iko kwenye mkakati wa kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji vyote nchi nzima hivyo wananchi wawe na subira watafikiwa na kwamba umeme huo mwananchi ataunganishiwa kwa Sh. 27000 tu na nguzo atawekea bure hata kama umbali wa kufika nyumbani utahitaji nguzo zaidi ya moja.
Aidha aliwataka wawekezaji waliochukua maeneo makubwa bila kuziendeleza kunyang’anywa na kurudishiwa wananchi ili waendelee na shughuli za uzalishaji na kwamba wale waliopewa maeneo na vijiji zaidi ya ekari 50 warudishe kwakuwa vijiji havina mamlaka ya kutoa maeneo zaidi ya ekari hamsini. Pia akizungumzia suala la maji Mh. Majaliwa alisema serikali inalifanyia kazi na kuzielekeza mamlaka za maji kuhakikisha wananchi wanapata maji ambayo ni salama na kuwaeekeza kubaini maeneo ya kuchimba visima vya maji ili wananchi waondokane na adha hiyo kutekeleza kampeni ya Mh. Raisi ya kumtua mama ndoo.
Alihitimisha kwa kuwataka watumishi wa umma kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa weledi na kwamba wanatakiwa kwenda vijijini kutatua kesho za wananchi badala ya kukaa maofisini siyo mpaka kiongozi wa serikali aje ndipo walete kero zao hususani kupitia mabango.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu pia alitembelea kiwanda cha kutengeneza unga wa mahindi kilichopo Kata ya Mkata Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
MWISHO.
Imeandaliwa na;
Paulina John
Kitengo cha Habari na mawasiliano Handeni DC.
Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa akizungumza na wananchi na wananchi wakimsikiliza
Waziri Mkuu Mh.Kasim Majaliwa akizungumza jambo na mwekezaji wa kiwanda cha kutengeneza unga wa mahindi baada ya kukagua
Mh. Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akisilikiza maelezo ya mwekezaji wa kiwanda cha kutengeza unga wa mahindi Mhandisi Mwambashi wa kushoto
Waziri wa madini Mh.Doto Biteko akisalimia wananchi
Naibu Waziri wa maji Mh.Jumaa Aweso akiwatoa hofu wananchi kwa kutatua kero ya uhaba wa maji safi na salama maji
Naibu Waziri wa kilimo Mh.Omary Mgumba akisalimia wananchi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martin Shigela akisema neno la ukaribisho wa Waziri Mkuu Wilayani Handeni
Mbunge wa Handeni Vijijini Mh.Mboni Mhita akiwasilisha changamoto za Handeni kwa Mh.Waziri Mkuu
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe akijibu maswali ya Mh.Waziri Mkuu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe akijibu maswali ya Mh.Waziri Mkuu
Wakurugenzi wa Handeni vijijini Bw. William Makufwe kushoto na Handeni Mji Bw.Keneth Haule kulia wakimskiliza Mh.Waziri Mkuu
Viongozi mbalimbali wakifuatilia mazungumzo ya Mh. Waziri Mkuu
Afisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Bi. Edina Katalaiya wa kwanza kulia akipokea maagizo kutoka kwa Mh.Waziri Mkuu
Watumishi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Mh.Waziri Mkuu
Wananchi wakitoa kero zao kwa Mh.Waziri Mkuu
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa