Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imepokea miche 4000 ya mbegu za korosho kutoka bodi ya korosho ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ya kuanzisha korosho kama zao la biashara.
Miche hiyo ya mbegu za Mikorosho zilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe na kukabidhiwa kwa Maafisa Elimu tayari kupelekwa kwenye Shule zao kwa ajili ya kwenda kupanda.
Akizungumza na Maafisa Ugani, Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari na Maafisa Kilimo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Gondwe alieleza kuwa, kwa muda mrefu Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imekuwa haina zao la biashara la uhakika na wakati huohuo kuna ukanda ambao unakubali kustawi kwa zao la korosho, hivyo ni muhimu kuchukulia zao hili kama zao la biashara bila kujali ni muda gani unachukua mpaka mavuno.
“korosho linakuwa ni zao la biashara Wilayani Handeni, ni mti ambao utasaidia kutunza mazingira pia, lengo ni kuongeza uchumi wa wananchi, kushirikisha wanafunzi kwenye elimu ya kujitegemea na kuhakikisha wanafunzi hawapati shida ya chakula hatimaye kuongeza kiwango cha uelewa na ufaulu kwa watoto wetu” alisema Mh. Gondwe.
Mh.Gondwe Aliongeza kuwa mbegu hizi zitasambazwa kwenye taasisi za elimu hasa kwa shule ambazo zipo ukanda wa korosho na hazikupata mbegu za mihogo au zilipata kwa kiwango kidogo, ili iwe rahisi kusimamia na kufanya mashamba darasa kwa jamii inayozunguka shule.
Mh. Gondwe Aliwataka Maafisa kilimo kuwaandikia barua zitakazowataka kusimamia na kutoa elimu ya kilimo bora cha zao la mikorosho maafisa ugani wote watakaohusika na upokeaji wa mbegu kwenye maeneo yao.
Kuhusu suala la masoko Mh. Gondwe aliwatoa hofu na kuwaeleza kuwa masoko ya korosho Tanzania yapo na bado ataendelea kutafuta masoko huku akiwaasa katika suala la uvunaji bora ambao utaanzia kwenye matunzo ya zao tangu kupandwa hadi kuvunwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh. Ramadhani Diliwa aliwaeleza wanachi kuwa wananchi wa Wilaya ya Handeni hawajachelewa kuanza zao hilo na kulima mazao mengine ya biashara huku akisisitiza upandaji wa miti ambao kwa wakati mwingine ni kutunza mazingira na kwa upande mwingine ni biashara.
“ Tuache kushikilia zao la mahindi kama zao kuu la Handeni, wananchi amkeni, limeni mazao mengine ardhi ya Handeni inarutuba ya kutosha na uwezo wa kustawi mazao mengine zaidi ya mahindi, mimi nina ekari zaidi ya 50 ambazo nimelima mazao mbalimbali na kupanda miti aina tofauti karibuni mje kujifunza ” alisema mwenyekiti.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Simon Mdaki alishukuru kupokea mbegu hizo na kuwataka Maafisa Kilimo, Wakuu wa Shule kusimamia ukuaji wa zao hilo kwa weledi ili kuweza kufikia lengo la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni katika kuondoa dhana potofu ya wananchi wa Wilaya ya Handeni kutegemea zao moja tu la mahindi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa