WILAYA YA HANDENI YAPOKEA VITAMBULISHO VYA AWAMU YA PILI.
Wilaya ya Handeni imepokea vitambulisho vya awamu ya pili ambapo imepokea vitambulisho 5000 na kugawiwa jana katika Shule ya Sekondari Handeni kwa Maafisa Watendaji wa Kata zote za Wilaya Handeni ili viwafikie wajasiriamali wadogo katika maeneo yote ya Wilaya Handeni.
Akizungumza katika kikao cha maelekezo ya kusimamia uuzwaji wa vitambulisho hivyo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwapongeza Watendaji hao kwa kufanya vizuri katika uuzaji wa vitambulisho awamu ya kwanza na kuwasihi kuongeza juhudi zaidi awamu hii ya pili kwa kumaliza kwa wakati.
Gondwe amewaasa watendaji kuhakikisha wafanyabiashara ambao hawalipi kodi wote wanapata vitambulisho na kusiwe na urasimu wa kugawa vitambulisho hivyo kwa kigezo cha mtu kukosa viambata vya kupata kitambulisho hivyo mtu akiwa na fedha apewe kitambulisho chake viambata apeleke baadaye na kwamba baada ya kutoa kitambulisho watendaji hao wahakikishe wanaweka kumbukumbu ya uuzwaji wa vitambulisho vizuri .
Aidha aliwataka Watendaji kuelimisha wafanyabiashara kwa kushirikiana na wataalamu walioko ngazi ya Kata baada ya kukaa kikao cha Kata juu ya unafuu wa kuchukua kitambulisho badala ya kutoa vitambulisho hivyo bila wafanyabiashara kutokuwa na uelewa wa kutosha wa matumizi ya vitambulisho hivyo.
Pia aliwaeleza Watendaji hao kutoa taarifa pale wanapokutana changamoto kwa uongozi ili kutatua haraka iwezekanavyo na kwamba kila ijumaa ya wiki watoe taarifa ya uuzwaji wa vitambulisho na hadi kufika tarehe 28/02/2019 vitambulisho vyote viwe vimeshauzwa.
Wakati huo huo Mh. Gondwe aliwataka Wakurugenzi kuwaandikia barua ya kuwaachisha kazi Watendaji wanaojitolea na kuwakaimisha watumishi wa Serikali ngazi Kata wakimemo Maafisa Ugani na mifugo kwani Watendaji wakujitolea wamekuwa wakitafuta maslahi yao binafsi badala ya kuitumikia Serikali.
Alihitimisha kwa kuwataka Watendaji kuweka masuala ya kilimo, Elimu, miradi ya Maendeleo na Vitambulisho kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya Kata.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Mwl. Boniphace Maiga aliwataka Watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuepuka rushwa kwani baadhi yao wamekuwa wakijihusisha na masuala ya rushwa na alisema endapo mtu atagundulika atachukuliwa hatua stahiki. Pia aliwataka watendaji kushirikiana kupekua miradi ya maendeleo iliyoko kwenye maeneo yao kwani kuna baadhi ya maeneo hawajui miradi iliyoko katika maeneo yao zaidi ya mtu aliyeko kwenye kituo cha mradi na kwamba jambo lolote likitokea ngazi ya Kata uongozi wa Wilaya ujulishwe mapema ili kurahisisha ufuatiliaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alisema lengo la Mh. Raisi ni kuwajengea watanzania utamaduni wa kulipa kodi na tozo mbalimbali ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ili kuondokana na utegemezi wa wafadhili kutoka nje na pia kupata takwimu ya wafanya biashara na aina za biashara pamoja na kuondoa ushuru ambao wanatozwa wafanyabiashara bila kufuata kanuni na sheria.
Pia aliwataka Watendaji hao kuwa na utamaduni wa kutekeleza maelekezo badala ya kulalamika au kupuuza kwani mara nyingi wakipewa maelekezo wamekuwa wakipuuza.
Aidha aliwataka Watendaji hao kuwafuata wajasiriamali waliko badala ya kuwasubiri maofisini ili kurahisisha ufanikishaji wa zoezi hilo na alitaja wajasiriamali wanaotakiwa kupewa vitambulisho ambao ni watu wenye mapato ghafi isiyozidi milioni nne kwa mwaka, ambao hawana TIN namba na ambao wana TIN namba lakini hawajalipa kodi kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni Bw. Keneth Haule alisema kuwa jambo lolote linaloamuliwa na mamlaka halali ni sheria hivyo aliwataka watendaji Kata washirikiane na viongozi wa ngazi ya Kata ili kukamilisha majukumu kwa pamoja na kwamba wasifanye kazi kwa udungu na mazoea bila kufuata sheria.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wa Handeni Bw. Kamuhanda alisema kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana uongozi wa Wilaya ili kufanikisha zoezi la uuzwaji wa vitambulisho lakini aliwaasa watendaji kutokuwalazimisha wafanyabiashara wenye leseni kuchukua vitambulisho kwani inaweza kuleta mkanganyiko wa taarifa za wafanyabiashara hao.
Watendaji wa Kata kwa pamoja waliafiki kufanya kazi kwa weledi na kwa moyo ili kufikia azma ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MWISHOO.
Mkurugenzi Mtendaji Handeni DC Bw. William Makufwe akitoa maelekezo
Mkurugenzi Mtendaji Handeni Mji Bw. Keneth Haule akitoa nasaha.
Katibu Tawala Wilaya Mwl.Boniphace Maiga akitoa neno la Ushauri kwa Watendaji Kata
Wajumbe wa kikao wakiomba kwaajili ya Afisa biashara (Charles) aliyepata ajali katika ugawaji wa vitambulisho vya awamu ya kwanza.
Watendaji Kata wakipokea Vitambulisho na kusaini kukiri kupokea vitambulisho hivyo
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa